Imeandikwa na Asha Haji , Pemba
Wananchi wa kijiji cha Kambini kwajuni Shehia ya kambini kichokochwe Wilaya ya Wete mkoa wa kaskazini Pemba wamesema, wanajisikia faraja kufikiwa na huduma ya maji safi na salama kwani muda mrefu waliishi pasi na kuwepo huduma hiyo.
Aidha wamelishuhukuru shirika na DIRICT AID (Africa Muslim Agency) kwa kujitolewa kuwachimbia kisima kijijini kwao wakisema kuwa kufanya hivyo kuna dhihirisha kuwa taasisi hiyo ina mapenzi ya dhati kwa wananchi.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi aliyefika kijiji kwao walisema, waliishi na dhiki kwa muda mrefu huku wakilazimika kwenda masafa marefu kufuata huduma hiyo lakini walisema , ingawa bado changamoto hiyo ipo lakini kwa kiasi fulani imetatuka baada ya kutokea wafadhili kuwajengea kisima hatimae wameanza kuneemeka.
Asha Mwinyi Hamad mmoja miongoni wanakijiji hicho alisema muda mrefu waliamua kupambana na hali hiyo hadi pale mradi wa kukuza uwajibikaji Zanzibar PAZA (Promoting Accountability of Zanzibar)ulipo wafikia kijijini mwao.
Alisema mradi huo ulikua na uhamasishaji mkubwa kwa wananchi juu ya kupigia mbio haki zao ikiwamo hiyo huduma ya maji , hivyo wananchi waliamua kuyafanyia kazi mafunzo hayo kwa kudai haki yao ya kupata huduma ya maji hatimae walifika hadi kwa wafadhili na kuwachimbia kisima.
Nae Siti Hamad Rashid alisema, wanawashukuru sana NGENARECO na wadau wenzao kuwaletea mradi huo kwani umewafanya wawe na uwezo wa kuzungumzia haki zao popote pale kwa mujibu wa sharia.
“lakini ingawa kisima kipo lakini hakitoshelezi kutokana na watu waliyopo, bado tunawaomba wahusika watufikirie, lakini tunashukuru kwa hapa tulipopata”alisema Siti.
Kwa upande wake Bakari Suleiman Juma ambae ni mwezeshaji wa wananchi kupitia mradi wa PAZA alisema, tokea wananchi kufikiwa na mradi huo kwa kiwango kikubwa wameamka kufuatilia haki zao kiasi ambacho mpaka walifika katika shirika la DIRECT AID na kuamua kuchimbiwa kisima.
Akielezea zaidi alisema, anatamani kuona mradi unaendelea ili wananchi wazidi kunufaika kwa kupata taaluma ya kujielewa katika kufuatilia haki zao
“kwakweli mradi umesaidia sana, wananchi wanaonekana kabisa wamenufaika” alisema mwezeshaji huyo.
Mradi huo umekuja kwa lengo la kukuza uwajibikaji katika majukumu hatimae kufikia mendeleao katika eneo husika na unaendeshwa na chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania –TAMWA upande wa Zanzibar , Jumuiya ya waandishi wa habari za Maendeleo Zanzibar – WAHAMAZA na NGENARECO – PEMBA chini ya mradi wa kuziwezesha asasi za kiraia Zanzibar, ZANSASP,ambapo mradio huo upo ikingono kumalizika na unatarajiwa mwezi wa Pili mwaka 2019