Tuesday, 29 January 2019

Idadi ya waliokufa kwa kula chakula chenye sumu yaongezeka Pemba



Idadi ya waliokufa kutokana na kula chakula kinachosadikiwa kuwa na sumu katika kijiji cha Shanake Kiuyu Mbuyuni Wilaya ya Micheweni, imeongezeka na kufikia sita baada ya mmoja miongoni mwa waliyokuwa wakipatiwa matibabu hospitali kufariki dunia siku ya Jumamosi.
Akizungumza Daktari wa zamu katika hospitali waliyolazwa ya Micheweni Dkt. Hamad Said Hamad, amemtaja mwengine aliyefariki ni
Chumu Sadiki Shoka (28) na kusema bado wagonjwa wengine wanne wanaendelea na matibabu.
Aliwataja wagonjwa hao kuwa ni  Asma Makame Ali (12), Rashid Sadi Khatib (10), Shajiya Kombo Shoka (25) na Chumu Shiba Faki, anayekisiwa kuwa na umri wa miaka 35.
“Mmoja wa wagonjwa waliokuwa wanapatiwa matibabu alifariki jana (juzi) ambapo kwa sasa tunaendelea kuwatibu wagonjwa wanne, ambao hali zao zinaendelea vizuri, isipokuwa Asma Makame Ali, hali yake sio nzuri sana,” alisema.
Wengine waliofariki dunia kutoka na tukio hilo, ni Hafidh Khatib Rashid, Hifidh Khatib Rashid ambao ni watoto mapacha, Fatma Khatib Ali, Sabra Said Rashid na Hamida Bakar Rashid.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wa habari hizi, walisema kwamba kwa kuwa waathirika hawajawa tayari kutaja aina ya chakula walichokula, ni vyema serikali kuharakisha uchunguzi.
Katika maelezo yao waathirika wa tukio wametofautiana kuhusu chakula walichokula, ambapo baadhi wanadai kwamba walikula dagaa,  wengine samaki aina ya  ngogo na kasa na baadhi yao walisema walikuwa wali kwa maharage.
Hivyo chakula kilichopelekea tatizo hilo bado hakijafahamika.

No comments:

Post a Comment