Naibu waziri wa kilimo Maliasili,Mifugo na Uvuvi Dk.Makame Ali Ussi akizungumza katika mafunzo ya siku tatu kwa wafugaji wa Samaki na watendaji wa sekta za mazao ya Bahari juu ya ufugaji wa Mazao ya baharini katika ukumbi wa kituo cha kuzalishia vifaranga vya mazao ya bahari Bet al ras Bububu wilaya ya Magharib A Unguja amesema serekali inatambua umuhimu wa rasilimali za bahari ambazo zinachangia kuengeza mapato ya nchi pamoja na kuwawezesha wananchi kujikwamua na umaskini.
Amesema serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wanaendelea na jitihada mbalimbali katika kutatua matatizo yanayowakabili wavuvi na wafugaji wa mazao ya bahari ikiwemo Majongoo,Samaki na Kaa.
Dk.Makame amesema wakati umefika kwa Sekta ya bahari kuendelea kuwa muhimili mkuu utakaochangia ukuwaji wa uchumi wa nchi pamoja na kuwawezesha wananchi kuwa na uhakika wa chakula.
Amesema takwimu za uzalishaji wa mazao ya baharini zinaonesha kuwa takribani asilimia 40 inawawezesha wananchi kunufaika na ajira ambapo asilimia 70 ya wananchi wanategemea sekta hiyo katika kujikwamua na umaskini jambo linachangia ukuwaji wa maendeleo nchini.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu anaeshughulikia mifugo na uvuvi Dk.Islam Seif amesema ili kuhakikisha Wavuvi na wafugaji wanafikia malengo waliyoyakusudia Wiizara itaendelea kushirikiana na wataalamu katika kutatua matatizo yanayojitokeza katika sekta hiyo.
Amesema mpaka sasa muitikio kwa wafugaji umekuwa mkubwa ambapo hadi kufikia Wavuvi 49 elfu kutoka 35 elfu jambo ambalo linachangia maendeleo ya Uchumi Nchini.
Ametowa wito kwa Wavuvi kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali na wadau wa maendeleo katika kuleta maendeleo pamoja na kuwa na matumizi mazuri rasilimali za bahari ili ziweze kuwanufaisha wananchi.
Mratibu wa kituo cha kuzalisha vifaranga vya Samaki Bet al ras Buriani Mussa amesema ni vyema kwa wananchi hususan vijana kuchangamkia fursa zilizopo za kujikita na ufugaji wa mazao ya baharini ili waweze kujingizia kipato cha uhakika.
Amesema si vyema kwa vijana kushindwa kushiriki katika miradi inayoanzishwa badala yake watafute njia mbada za kuweza kujiajiri na kuachana na mawazo ya kusubiri ajira kutoka serikalini.
Washiriki wa mafunzo hayo Naima Ibrahim na Semen Muhammed wameomba kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili waweze kuzalisha mazao ya bahari yanayoendana na mahitaji ndani na nnje ya nchi.
Wamesema mbali na mafunzo pia ni vyema kwa wasimamizi wa kituo cha kuzalisha vifaranga vya mazao ya bahari kufanya kazi kwa uhakika ili waweze kufikia malengo waliyoyakusudia ikiwemo kuondoa tatizo la upatikanaji wa vifaranga kwa wafugaji.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kudumu kwa siku tatu kwa lengo la kuwafunza wafugaji na wasimamizi wa mazao ya baharini namna bora ya kuimarisha ufugaji wa mazao hayo umekutanisha pamoja Wafugaji ,Wataalamu wa Masuala ya Bahari na Watendaji wa Wizara ya kilimo chini ya ufadhili wa FAO na KOICA pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment